Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, chombo kimoja cha habari cha Yemen kimechambua, katika makala yake, madai ya Saudi Arabia kuhusu kuilinda Makka na Madina, pamoja na tuhuma zake dhidi ya Ansarullah kwamba inatishia maeneo matakatifu, na kuyalinganisha na mashambulizi yanayofanywa dhidi ya misikiti nchini Yemen.
Kauli rasmi za vyombo vya habari vya Saudi Arabia zimekuwa zikijikita daima katika suala la kulinda maeneo matakatifu ya Kiislamu, hususan Makka na Madina. Riyadh mara kwa mara imekuwa ikidai kuwa maeneo hayo yanatishiwa, huku ikiishutumu Harakati ya Ansarullah kuhusika na vitendo hivyo na kujitambulisha kuwa mtetezi wa Misikiti Miwili Mitakatifu.
Hata hivyo, madai hayo yanapolinganishwa na hali halisi iliyopo kwenye uwanja wa mapambano, swali zito na lisiloweza kupuuzwa linajitokeza: Inawezekanaje mtu kudai kuwa anailinda Makka, wakati misikiti ya Yemen inakabiliwa na mashambulizi ya mabomu?
Matumizi ya mara kwa mara ya suala la maeneo matakatifu katika mazungumzo ya kisiasa ya Saudi Arabia yanaweza kuchukuliwa kuwa ni juhudi za kutaka kuungwa mkono na Waislamu, pamoja na kujipatia uhalali katika mgogoro tata wa kisiasa na kijeshi. Wakati wa vita, pande zinazohusika wakati mwingine hutumia alama na nembo za kidini ili kupata maoni ya umma na kuhalalisha misimamo yao. Hata hivyo, madai hayo hukabiliwa na changamoto kubwa pale yanapokosa kuendana na ushahidi na hali halisi iliyopo kwenye uwanja wa mapambano.
Sehemu kubwa ya ukosoaji inaelekezwa kwenye mkanganyiko huo. Mgogoro wa Yemen ni suala linalohusiana na mamlaka na ardhi ya nchi hiyo, na maeneo matakatifu ya Kiislamu, yakiwemo Makka na Madina, pia yana nafasi maalumu na heshima isiyopaswa kuvunjwa kwa Waislamu wote wa Yemen.
Lakini mkanganyiko mkubwa zaidi unaonekana katika tofauti kati ya kauli na vitendo; ambapo katika kipindi cha chini ya wiki mbili, zaidi ya misikiti saba nchini Yemen imelenga kwa mashambulizi ya kijeshi!
Misikiti saba! Si kambi za kijeshi, si maghala ya silaha, wala si vituo vya makamanda; bali ni Nyumba za Mwenyezi Mungu, ambapo sauti za adhana husikika, waumini humuabudu Mwenyezi Mungu na kusujudu kwa kuweka paji za nyuso zao ardhini.
Kuharibu au kusababishia madhara misikiti na kubomoa Nyumba za Mwenyezi Mungu ni kuvunja heshima ya maeneo ambayo utukufu wake umesisitizwa katika mafundisho ya Mwenyezi Mungu na pia katika sheria za kimataifa za kibinadamu.
Mtu anayebomoa misikiti huku waumini wakiwa ndani yake anawezaje kudai kuwa anautetea Uislamu? Na inawezekanaje kugeuza Nyumba za Mwenyezi Mungu kuwa magofu, huku wakati huohuo ukipeperusha bendera ya kutetea Misikiti Miwili Mitakatifu?
Hapa ndipo mkanganyiko mkubwa wa kimaadili unapojitokeza: Inawezekanaje mfumo mmoja wa kisiasa kudai kuwa unalinda maeneo matakatifu ya Kiislamu na kuwa na mamlaka ya uangalizi juu ya Haram Mbili Takatifu, lakini wakati huohuo ukaonyesha mwenendo wa namna hiyo mbele ya uharibifu wa maeneo ya ibada nchini Yemen?
Mantiki ya kimaadili inataka kwamba kila anayejidai kulinda Nyumba za Mwenyezi Mungu aheshimu utukufu wa misikiti na maisha ya raia wasiohusika katika sehemu zote za dunia; badala ya kutofautisha heshima ya eneo takatifu lililoko Makka na heshima ya msikiti pamoja na waumini wake nchini Yemen.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Aya ya 114 ya Surat Al-Baqara:
﴿وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنْ مَنَعَ مَسَاجِدَ اللَّهِ أَنْ يُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ وَسَعَىٰ فِي خَرَابِهَا﴾
“Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayezuia jina la Mwenyezi Mungu kutajwa ndani ya misikiti Yake na akajitahidi kuibomoa?”
Kwa mujibu wa Aya hii, kujitahidi kubomoa misikiti na kuzuia ibada ya Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa aina kubwa za dhuluma. Kwa kipimo hicho, inawezekanaje mtu kudai kuwa analinda maeneo matakatifu ya Kiislamu, huku akiwa hajali uharibifu wa Nyumba za Mwenyezi Mungu nchini Yemen?
Haiwezekani tena kuwashawishi wananchi kwa kutumia kauli mbiu zinazovutia na maneno ya hisia ambayo hayana uhusiano na hali halisi iliyopo kwenye uwanja wa mapambano. Watu wanapima vitendo sambamba na madai, na kile kinachotokea kwenye misikiti nchini Yemen kinazua maswali mazito kuhusu madai ya kulinda maeneo matakatifu ya Kiislamu.
Misikiti iliyobomolewa itajengwa tena, na kumbukumbu za waumini waliopoteza maisha yao katika mashambulizi hayo zitabaki katika fikra za wananchi. Hata hivyo, madai ya kulinda Makka na Madina hayawezi kuendelea milele bila kuwajibishwa kuhusu yale yaliyotokea katika misikiti ya Yemen.
Mtu ambaye haeshimu hata msikiti mdogo katika kijiji kimoja nchini Yemen, anawezaje kudai kuwa analinda Msikiti Mtakatifu wa Makka (Al-Masjid al-Haram)?
Chanzo: Ufuq News – Yemen
Maoni yako